Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawezi
kulumbana na viongozi wa chama chake cha zamani cha Chadema kwa kuwa
anachofanya sasa ni kutafuta wanachama wa chama chake kipya.
Zitto alisema hayo juzi mjini Morogoro wakati wa
mkutano wa ziara ya uzinduzi wa chama hicho uliofanyika katika kiwanja
cha ndege mjini hapa.
Akihutubia huku akishangiliwa na wananchi, Zitto
aliwataka kumpima na kumchuja yeye kwa matendo yake na kwamba kwa sasa
jitihada zake amezielekeza mikoani kupata wanachama.
“Nimekuwa nikisikia maneno maneno mengi kutoka kwa
viongozi wangu wa zamani lakini nawaheshimu na sitoweza kuwajibu kwani
siasa za chuki kwa sasa zimepitwa na wakati, ninachofanya ni kukijenga
chama,”alisema Zitto.
Kiongozi huyo alisema Morogoro ni moja ya mkoa
unayoifanya nchi kukosa maendeleo kutokana na viwanda vingi
kubinafsishwa na hivyo kutokuwa na faida kwa wananchi.
“Morogoro ni mkoa wa sita katika kuchangia pato la
Taifa na takribani Sh2.2 trilioni zimekuwa zikipatikana kwa ajili ya
maendeleo ya watu wa mkoa huo,” alisema Zitto.
Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira aliwataka
wanawake nchini kuacha kushiriki siasa za vurugu na malumbano hasa
katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mghwira alisema ni vyema wakaangalia namna gani
nchi inakua kiuchumi na watoto na vijana wanapata elimu iliyo bora
ambayo itawafanya kufanya kazi kwa uzalendo.
Aliwataka wananchi kuwa na taratibu za kuwakumbuka
mashujaa wa Taifa hasa kwa mambo mema na mzuri waliyoyafanya wakati wa
uhai wao.
Mpaka sasa chama hicho cha ACT kimefanya mikutano
yake ya uzinduzi katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa na Morogoro na Dodoma .
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.