Baada ya tuhuma hizo kuelekezwa kwake na gazeti la Taifa Imara
lililochapishwa Machi 23, mwaka huu likiwa na kichwa cha habari
kinachosema, ‘Zitto amchongea Mengi kwa JK? Mwenyewe ameibuka Dar es
Salaam jana na kuzikanusha mbele ya waandishi wa habari akisema
zimemshtua na kumuogopesha.
“Tuhuma zilizotolewa na gazeti la Taifa Imara la Machi 23-29, mwaka
huu kwamba nina nia ya kutaka kuiangusha Serikali ya Rais Kikwete na
kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, zimenishtua
sana,” alisema Mengi.
Alisema habari hiyo imempa hofu kubwa juu ya mustakabali wa maisha
yake kutokana na kile kilichoandikwa kuwa Kikwete aliapa atapambana
naye.
“Hofu yangu kubwa inasababishwa na Ikulu na Maelezo kwa kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi.
“Ikulu na Maelezo wako makini katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa
jambo lolote linalomhusu Rais Kikwete, lakini katika hili nashangaa
kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,”
alisema Mengi.
Alisema hofu yake inazidi kuwa kubwa zaidi kwa sababu Kikwete ni Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, hivyo kauli yake kama ilivyonukuliwa
na gazeti hilo atapambana naye inaweza kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo
vya dola na kumuangamiza.
Pamoja na mambo mengine, habari hiyo ilisema Zitto Kabwe amemchongea
Mengi kwa Kikwete kuwa ndiye kinara wa kuhujumu Serikali yake.
Habari hiyo iliyoeleza kuwa chanzo chake ni Ikulu, iliendelea kudai
kuwa Zitto alikutana na Kikwete muda mfupi baada ya kuwasilisha bungeni
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu kashfa ya
Akaunti ya Tegeta Escrow wakati huo akiwa ni mwenyekiti.
Habari hiyo ilidai katika mazungumzo yake na Kikwete, Zitto
alinukuliwa akimueleza kuwa anayesababisha Serikali yake iyumbe mara kwa
mara ni Mengi.
“Zitto amekuwa akishawishiwa na Mengi kuiangusha Serikali ya Kikwete
na alikwenda mbali zaidi kumwambia rais kwamba, Mengi ameapa kuwa
kiongozi huyo akimaliza muda wake wa urais atamshughulikia kwa nguvu
zake zote,” ilisema sehemu ya habari hiyo.
Habari hiyo ilisema baada ya maelezo hayo, Kikwete aliapa kupambana na Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa taarifa hizo.
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.