Mchaka Zaidi

Sunday, April 19, 2015

Watanzania Hatarini Ghasia za Afrika Kusini

Watanzania wanaoishi Afrika Kusini, wako hatarini kutokana na vurugu zinazofanywa na wenyeji wa nchi hiyo, dhidi ya wananchi wengine wa asili ya Afrika wanaoishi nchini humo.

Akizungumza na mwandishi jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi, Mkumbwa Ally, alisema Mtanzania mmoja amechomewa duka lake, huku wengine 15 wakiwa katika kambi maalumu, wakisubiri msaada wa kurejeshwa nyumbani.
 
Kwa mujibu wa Mkumbwa, Ubalozi wa Tanzania unaendelea kukusanya takwimu za Watanzania wanaoishi nchini humo na Serikali ya nchi hiyo imeandaa kambi maalumu za kuhifadhi wageni wakiwemo Watanzania, ambao wamekuwa wakifanyiwa fujo na watu wa nchi hiyo.     
 
“Hao Watanzania 15 ni wale ambao wako tayari kurudi nyumbani, sasa hivi Serikali inashughulikia utaratibu wa kuwarejesha nyumbani.
 
“Kuna dalili idadi ya walio tayari kurudi nyumbani ikaongezeka maana inasemekana vurugu, mbali na kufanyika katika mji wa Durban, sasa zinatarajiwa kuendelea katika jiji la Johannesburg,” alisema Mkumbwa.
 
Alisema hali hiyo inatia wasiwasi na Tanzania inatarajia Serikali ya nchi hiyo, itachukua hatua zinazotakiwa kuhakikisha usalama kwa Watanzania na watu wa nchi zingine, wakati Serikali ya Tanzania ikijiandaa kuwarejesha nyumbani wote watakaokuwa tayari.
 
Tayari taarifa kutoka katika mitandao mbalimbali ya habari, zimeonesha kuwa zaidi ya wageni 2,000 wenye asili ya Afrika wanaoishi nchini humo, wamewekewa kambi katika Uwanja wa Mpira wa Rydalvale, kwa ajili ya usalama wao.
 
Mmoja wa maofisa kutoka Ofisi ya Meya wa Durban, Sipho Mthethwa, amenukuliwa akisema wageni wengi wamepoteza mali zao na wana hasira na kazi aliyonayo ni kuwashawishi wapunguze hasira na anafanya hivyo kwa utaratibu.
 
Kwa sasa wageni hao wako katika makambi ambako kumewekwa maturubai huku wakihudumiwa na mashirika ya misaada.
 
Mthethwa alisema zaidi ya mabasi 24 yanatumika kusafirisha wageni hao kwenda katika kambi hizo, lakini tatizo wengi wamekuwa wakitaka kubeba mali zao na kukaa nazo katika makambi, huku familia zikitaka kuwa pamoja.
 
Alisema hali hiyo inamuwia vigumu, kwa kuwa taratibu za kambi za dharura, wanawake lazima wakae eneo tofauti na wanaume na mali zao zitafuata baada ya waathirika hao kupata eneo na kutulia.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.