Mchaka Zaidi

Friday, April 17, 2015

Tamko la Waziri Chikawe Kuzifuta Taasisi za Kidini na Kiraia Zinazojihusisha Na Siasa Lapingwa Kila Kona.......Yadaiwa ni Udikteta na Aibu kwa Demokrasia


Wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi katika maeneo mengi nchini, wamepinga vikali tishio la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, la kuzifuta taasisi za kijamii na kidini na kueleza kuwa amekurupuka, hakushauriwa na kushindwa kufuata misingi ya demokrasia na Katiba ya nchi.


Wakizungumza na Gazeti  la  Nipashe, wadau hao walidai kuwa, kufanya hivyo ni kusababisha vurugu na udikteta mkubwa kwa nchi inayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora na demokrasia.

Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec) na Askofu wa Jimbo la Rulenge, mkoani Kagera, Severin  Niwemugizi, alisema amelipokea tamko hilo kama matamshi ya watu ambao hawajakomaa kisiasa, wasio tayari kupokea maoni ya wengine tofauti na yao na kwamba halina haki bali limejaa woga.

“Katika nchi ya demokrasia yenye viongozi wa namna hii hawana tofauti na madikteta, ukianza kutishia wenzako kuwa ukisema maneno nisiyoyapenda nakufuta huo ni udikteta,” alisema na kuongeza:

“Sheria ya kura ya maoni inasema kutakuwa na makundi ya ndiyo na hapana, najiuliza ni kundi lipi la pande hizo, kwanini wawepo wanaozuiwa wasihamasishe watu kusema hapana kama taasisi za serikali zinazoruhusiwa kuhamasisha ndiyo?” alihoji.

Arusha: Ni  Udikiteta
Baadhi ya asasi za kijamii na watu binafsi mkoani Arusha, walisema tishio hilo ni udikteta ambao ni aibu kutolewa na viongozi katika nchi inayothamini demokrasia na kwamba inapaswa kukemewa kwa vile ina lengo la kupora uhuru wa kujieleza ambao upo kikatiba.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Utetezi wa Haki za Wafugaji, Warina Asali na Waokota Matunda (Pingo’s Forum), Edward Porokwa, alisema kauli ya Waziri Chikawe ni tishio kubwa linalowanyima uhuru wa kujieleza.

“Kweli kauli hii ni tishio kubwa na tunapaswa kuikemea, sababu inatunyima haki na uhuru wa kujieleza kwenye masuala yetu yanayotuhusu kama katiba pendekezwa,” alisema.

Mkurugenzi wa asasi ya Grassroot Youth Development Organisation (GYDO), Henry Cigwasi, alishauri matamko mengine ya viongozi wa serikali yatolewe baada ya kufanyiwa utafiti.

Alisema maisha yote ya binadamu ni siasa, kila kitu anachofanya ni siasa, hivyo hawawezi kuacha kuzungumzia au kutoa elimu ya uraia bila kuzungumzia masuala muhimu yanayohusu maisha yao.

Alisema huku akitoa mfano wa Katiba Inayopendekezwa, kuwa wapo viongozi serikalini ambao wamesikika mara kadhaa wakiwahamasisha wananchi kuipigia kura za ndiyo siku ya kupiga kura ya maoni itakapowadia.

Lakini alisema wapo watu ambao wameichambua Katiba hiyo na kutoa maoni tofauti na viongozi wa serikali, lakini kwa kuwa maoni yao yanakinzana na viongozi wa serikali, wananyamazishwa.

“Kama kuna asasi au taasisi ya dini inatoa elimu kuonya kuhusu ubaya wa kitu fulani, tatizo lipo wapi hapo,” alisema.

Alishauri viongozi wa serikali kabla ya kutoa matamko kuhusu jambo fulani la kitaifa lililotokea basi ni vema kama kungekuwa na majadiliano ya kitaifa na wadau wahusika mapema ili kuepusha kutokea kwa vurugu au shida katika jamii.

Mkazi wa Sakina, Samuel Mollel, alisema hauli hiyo ikitekelezwa italeta vurugu kubwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Dr. Bana: Waziri  Kakurupuka
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema inaonyesha waziri alikurupuka bila kushauriana na kwamba siyo kauli inayopaswa kutolewa kwa umma katika zama hizi za demokrasia na siasa huria.

“Amekosea, ninachojua serikali haiwezi kufuta Katoliki au KKKT, utajiridhisha umewafutia, lakini dini itaendelea kuwapo, askofu hawezi kufuta ukatoliki wangu, hayo yanatokea kwenye mataifa yenye udikteta pekee,” alisema.

Alisema kwa kipindi hiki ambacho waziri alipaswa kusisitiza ni vyama hivyo kuzingatia masharti ya uandikishaji wake bila kutaja siasa.

“Kuanza kusema utavifuta wakati unaona kuna tamko la maaskofu ambalo bado lipo hai ni kujikanganya…akija kwa visivyofuata sheria na Katiba atafikiriwa vibaya,” alisema na kuongeza:

“Ninachoona waziri ali ‘over step’ hakujiridhisha, ndiyo maana serikali zote zinakuwa na msemaji mmoja na siyo kukurupuka, ukishasema unafuta taasisi za dini ni hatari…natoa ushauri wa bure kwa serikali yangu,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar  es Salaam, Bashiru Ally, alisema: “Jukumu kubwa la serikali yoyote ni katika ‘law and order’ na ‘stability’, lakini serikali ya kidemokrasia haitumii mabavu bali unaweza kujenga amani na utulivu kwenye nchi kwa kujadiliana,” alisema.

Alisema kama zipo sababu za msingi ni vyema mahakama ikatumika kuthibitisha tuhuma zozote kwa kuwa ndicho chombo cha kikatiba chenye uwezo wa kitaalamu wa kusikiliza na kwamba kufuta hivi hivi ni kurudi katika utawala wa kiimla.

THRDC: Tanzania  ya Sasa  Siyo  ya  Zamani
Mtaribu wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania  (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema viongozi wawe makini na kutambua kuwa Tanzania ya sasa siyo ya zamani na kwamba wanapoona mambo hayaendi lazima wazungumze.

Alisema asasi na viongozi wa dini wana wajibu kwenye masuala yote kwa kuwa walishirikishwa kwenye mchakato na Bunge la Katiba, hivyo kwa sasa wanapoona mambo hayako sawa wanapaza sauti.

Alitolea mfano suala la uandikishaji wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa BVR na mchakato wa kura ya maoni yalikuwa hayakwepeki kuzungumzia kwa kuwa amani ya nchi inategemea masuala yote hayo.

Dodoma:Chikawe  Asitumie  Vibaya  Nafasi  Yake
Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya, alisema Waziri huyo asitumie nafasi yake kuchafua zaidi ila kama ni kumsaidia basi Mungu ambariki na wanamuombea.

"Kama atafuta kwa mujibu wa sheria na taratibu na si kama analipuka, atatekeleza kazi yake kwa usahihi, lakini  akilipuka  anaweza kuleta athari kubwa,” alisema.

Alisema hofu yake ni kusiwe na hasira na zikaelekezwa kwa watu wasio na hatia.

"Viongozi wa dini tuna haki  kuelekeza watu kitu gani tunachokifikiri ambacho ni sahihi kwa hiyo kama kuna mtu akitokea akaona ni uasi au si uasi ila na sisi pia tumepewa majukumu ya kumwambia mtu afanye kitu gani ambacho ni sahihi,” alifafanua.

"Hebu tujiulize kwanini huko nyuma haikuwa hivi kwanini hizi hoja kwa sasa zinajitokeza, kwanini leo hii viongozi wa dini wafike kutoa kauli hiyo je, walikuwa ‘right’ au ‘wrong’, haya yanatakiwa kufanyiwa utafiti na ni utafiti rahisi sana,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) mkoa wa Dodoma, Kayumbo Kabutari, alisema Chikawe anadanganya wananchi, nchi haiko salama.

Maaskofu: Tunasubiri  Waraka  wa  Serikali
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Kanda ya Kaskazini na Kati, Christopher Madilu, alisema tamko ni gumu kueleweka kwa sasa, ingawa viongozi wa dini pamoja na kanisa hilo wanasubiri waraka wa serikali ili watoe msimamo wao.

“Kuna ugumu wake katika kuzungumzia utekelezaji wa tamko la Waziri Chikawe. Sisi tunasubiri waraka wa serikali unaoonyesha kusudio hilo, halafu ndiyo tuzungumze ya kwetu. Lakini mpaka sasa hakuna waraka ulioletwa, inawezekana labda serikali imechunguza na ikaona kuna makosa, hatuwezi kujua kwa hiyo tunasubiri,” alisema Askofu Madilu.

Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, alisema hawana taarifa na wanasubiri waraka wa serikali.

Prof. Willy Makundi ambaye ni mtaalamu wa mabadiliko ya tabia nchi, alisema anashangazwa na tamko hilo wakati nchi inaongozwa kwa misingi ya sheria na Katiba.

“Hata kama kungekuwa na mtu au kikundi cha watu au taasisi ya dini imevunja sheria, serikali haina nguvu ya kikatiba na ya kiutekelezaji kuyafunga makanisa, isipokuwa mahakama peke yake, kwa sababu ndiyo dalali mkuu wa haki…hakupaswa kutoa vitisho na badala yake angeagiza waburuzwe mahakamani,” alisema Prof. Makundi

Tanga: Serikali  Iache  Vitisho
Baadhi ya wadau wa masuala ya maendeleo mkoani Tanga wameitaka serikali kuacha kutoa vitisho kwa raia wake kwani ni kukiuka Katiba ya nchi kuhusiana na uhuru wa wananchi wa kutoa maoni yao bila kuingiliwa.

Walisema kauli hiyo inaweza kuchangia kusababisha vurugu ndani ya nchi hasa kwa serikali kutaka kutumia mabavu kufanya maamuzi ambayo hayakubaliki, jambo ambalo ni kinyume cha misingi ya utawala bora.

“Utawala bora ni ule unaofuata misingi ya haki na sheria kwa mujibu wa Katiba ya nchi, kama Katiba inayotumika sasa inatambua uhuru wa mwananchi wa kutoa maoni bila kuingiliwa iweje serikali ione ni kosa la jinai,” alisema Mbone Herman, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria (OUT).

Mariam Said, mkazi wa jijini Tanga, alisema kauli ya serikali inatokana na ukweli kwamba Katiba inayopendekezwa si maoni na mahitaji ya Watanzania, bali ni pendekezwa kwa ajili ya kuwalinda baadhi ya waliopo madarakani.

Mnyika: Nitapeleka  Hoja  Bungeni
Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, John Mnyika, alisema Chikawe angewambia ukweli vyama wanavyotaka kuvifuta ni ambavyo walitangaza kwenye vyombo vya habari na siyo vilivyotoa msimamo katika kura ya maoni na uchaguzi mkuu.

Alisema iwapo vyama hivyo vitafutwa kwa kisingizio hicho atapeleka hoja bungeni lijadiliwe na waziri awajibishwe.

“Namtaka waziri asijiingize kwenye hatari ya kupelekewa hoja ya kukiuka haki ya kikatiba ya watu kitaasisi kutoa maoni, kama ni suala la watu kutimiza masharti ya kisheria asifute, akifuta nasi tunakwenda kumfuta bungeni,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo.
 
“Amekurupuka akasome vizuri Sheria ya Kura ya Maoni ajue ni haki ya watu kushiriki kampeni na kama kura ingekuwa Aprili 30, mwaka huu, kungekuwa na kampeni za ndiyo na hapana,” alisema.

Alisema kauli ya Chikawe na nguvu aliyotumia siyo kura ya maoni pekee, bali wamegundua asasi, taasisi na watu wanataka mabadiliko hawakubaliani na mfumo wa utawala, wanatoa lugha za ukali kuwatisha, kuwaziba midomo kuelekea watu kusaka mabadiliko.

Alisema wanaosababisha kuvunjika kwa amani ni uongozi dhaifu unaoshindwa kusimamia ufisadi na kwamba kinachoonekana kwa sasa ni kuporomoka kwa hali ya maisha ya wananchi na tofauti kubwa kati ya maskini na tajiri ambalo ndilo tishio kubwa.

Kanda  ya  Ziwa  Wamshangaa  Chikawe
Wakazi wa Shinyanga, walisema tamko la Chikawe ni la kukurupuka kutokana na Katiba ya nchi kusema kila mtu ana haki ya kutoa maoni na mawazo yake bila kuvunja sheria za nchi.

Hassani Baruti, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Shinyanga Mjini, alisema Chikawe amevunja Katiba ya nchi kwa kuingilia uhuru wa mtu binafsi na haiwezekani kuzuia watu kutoa maoni.

Mwanaharakati wa siasa mjini Shinyanga, Saguda Komanya, alisema kila nchi ina miongozo yake na katika suala la Katiba inayopendekezwa kila mtu ana wajibu wa kuikosoa na kuitolea maoni.

Komanya alisema suala la hofu ya amani kuelekea uchaguzi mkuu halipo isipokuwa Jeshi la Polisi linatakiwa lisiegemee upande wa chama chochote zaidi ya kutenda haki.

 Mkoani Simiyu, baadhi ya asasi zimeleeza kushangazwa na tamko hilo na kulitiliwa hofu.

 Mwenyekiti wa mtandao wa asasi za kiraia wilayani Maswa, Nicodemas Lutta, alisema kitendo cha Chikawe kutoa tamko hilo ni kuwanyima wananchi pamoja na asasi zao haki ya kidemokrasia ya kuamua mambo nchini.

Alisema kuzifungia asasi za kiraia na kidini kuna utaratibu wake, na kumtaka Chikawe atoe ushahidi wa asasi zinazotuhumiwa kuliko kujumuisha asasi zote hususani zile za kidini.

Lutta alisema haiwezekani kutenganisha siasa na dini na kuhoji serikali imekuwa ikiwahimiza viongozi wa madhehebu ya dini kuhubiri amani na upendo hasa kuelekea uchaguzi mkuu na kuwahimiza wananchi wao bila kujali imani zao za kidini kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa.

“Kwanini nawakataza wasihamisishe kupigia kura ya hapana wakati Katiba ni ya wananchi?” alihoji.

 Wilayani Chato baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini, walisema ni lazima kauli hiyo aifute kwani inaweza kusababisha machafuko.

“Chikawe lazima atambue viongozi wa dini ni walinzi wakubwa wa amani nchini, hivyo kitendo cha kuwataka kuwazuia kutoa maoni yao wakati muelekeo wa nchi unaenda mrama hakiwezekani,” alisema mchungaji wa kanisa Anglikana Chato, Zacharia Samson.

Katibu wa Chadema wilayani Chato, Mange Ludomya, alisema Chikawe amekiuka katiba ya nchi kwa kumkataza mtu kutoa maoni yake bila kuvunja sheria za nchi.

“Hivyo ni vitisho ili kuwafanya wananchi waikubali Katiba inayopendekezwa isiyoonyesha dira kwa Watanzania katika miaka 50 ijayo,” alisema Emmanuel Magida mkazi wa Igoma, jijini Mwanza.

Edward Mboje mdau wa asasi za kiraia, alisema waziri huyo hakutumia busara katika tamko lake hilo kwani asasi siyo serikali bali ni wananchi, hivyo haina haja kutoa kauli inayowanyima wananchi haki ya kutoa maoni kwa mambo ya kisimingi.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.