Kizungumkuti
kimezidi kujitokeza katika suala la kufungwa kwa shule za sekondari za
bweni za serikali kwa kile kinachoelezwa ni ukosefu wa chakula kutokana
na wazabuni kugoma, baada ya serikali kutoa tamko ikieleza kuwa kuwa
imelipa fedha za wazabuni hadi Machi, mwaka huu.
Katika
tamko hilo, serikali inazikana taarifa zinazotolewa na baadhi ya wakuu
wa shule hizo kuwa zinakabiliwa na uhaba wa chakula na kulazimisha
kuzifunga.
Hata
hivyo, licha ya kukana taarifa za wakuu wa shule zilizoathirika,
serikali inathibitisha kuchelewa kutolewa kwa fedha za chakula za Machi,
mwaka huu, ambazo zilipaswa kulipwa shuleni mwishoni mwa mwezi huo na
kwamba kwa sasa zipo kwenye akaunti za halmashauri.
Kutokana
na hali hiyo, serikali imewaomba wazabuni hao kuendelea kutoa huduma
wakati serikali inafanya utaratibu wa kuwalipa fedha hizo ambazo
zimeshafika kwenye akaunti za shule.
Kauli
ya serikali imetolewa siku chache, baada ya baadhi ya wakuu wa shule
hizo kueleza kuwa wameshindwa kuwaweka wanafunzi shuleni bila chakula na
kuwataka kurudi nyumbani hadi chakula kitakapopatikana.
Katibu
Mkuu wa Tamisemi, Jumanne Sigini, akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, aliagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa
na Majiji kuwachukulia hatua walimu hao kwa kuwa hawakustahili
kutangaza kufungwa kwa shule, bali kuwasiliana nao (wakurugenzi) ambao
ndiyo wenye mamlaka.
“Ninaposikia
mtu anasema tumekosa chakula tunafunga shule napata shida, haiwezekani
fedha ziende kwenye akaunti zao halafu wazabuni waseme hawajalipwa,” alisema.
Alifafanua
kuwa kwa kipindi cha Julai, mwaka jana hadi Machi, mwaka huu, serikali
imelipa zaidi ya Sh. bilioni 28.1 (asilimia 66.7) za chakula kwa shule
za sekondari za bweni, shule za msingi elimu maalum za bweni.
Alisema
kwa mwaka 2014/15 fedha zilizotengwa kwa ajili ya chakula ni zaidi ya
Sh. bilioni 42.1 na kwamba kiasi ambacho hakijalipwa ni zaidi ya Sh.
bilioni 13.9 ambazo ni (asilimia 33.23) za kumalizia miezi minne
iliyobaki.
Katibu
Mkuu huyo aliweka bayana mchanganua huo na kiasi cha fedha ambacho
kililipwa kwa kila mwezi kwenye mabano kuwa ni Julai (Sh. bilioni 3.5),
Septemba (bilioni 3.5), Oktoba (bilioni 3.5), Novemba (bilioni 2.1),
Januari (bilioni 3.5), Februari (bilioni 3.5) na Machi (bilioni 8.4).
Sagini
alisema zipo taarifa za kufungwa kwa baadhi ya shule na mikoa yake
kwenye mabano ambazo ni Rugambwa, Kahororo, Nyakato, Ihungo (Kagera);
Lyamungo (Kilimanjaro); Mpwapwa na Abeid Karume (Dodoma) na Kazima,
Milambo, Tabora Wasichana na Wavulana, (Tabora), kwa madai ya kukosa
chakula.
“Napenda
kutumia nafasi hii kuweka bayana kuwa wenye shule za sekondari ni
mamlaka za serikali za mitaa ambazo watendaji wake wakuu ni wakurugenzi.
Wakuu wa shule ni viongozi wasimamizi hawana mamlaka ya kutangaza
kufunga shule kwa sababu yoyote bila kibali cha mwenye shule. Wakati
wowote kunapotokea changamoto za uendeshaji wanatakiwa wafanye
mawasiliano na wakurugenzi wa Halmashauri,” alisema na kuongeza:
“Ikumbukwe
kuwa shule huendeshwa kwa vipindi maalum na kutokana na miongozo
iliyopo, mwanafunzi anatakiwa kusoma darasani siku 194 kwa mwaka, kwa
vyovyote vile idhini ya kufunga shule kabla ya tarehe zilizopagwa katika
muhula, inatakiwa kutolewa na Katibu Tawala wa Mkoa baada ya maelekezo
ya Katibu Mkuu Tamisemi.”
Katibu
Mkuu huyo alisema hadi sasa serikali haijatamka kufunga shule na kwamba
wakuu hao wamefanya makosa kwa kuwa hawakuwasiliana na mamlaka husika
ili kupata kibali, na kama kungekuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari, waliotaka kujua kama Tamisemi
imefuatilia kujua fedha hizo ziliingia kwenye akaunti za shule husika,
kiasi cha madeni ya nyuma ya wazabuni, idadi ya wazabuni na lini madeni
hayo yatalipwa, Sigini alisema wamezungumza na wakurugenzi wa
halmashauri husika ambao wamedai kupeleka fedha kwenye shule husika na
kwamba Wizara inafuatilia kama fedha hazikupelekwa Wakurugenzi
watachukuliwa hatua stahili.
Kuhusu
madeni ya miaka ya nyuma ya wazabuni, Sigini alisema hawana kumbukumbu
sahihi kwa wakati huu, lakini ni kweli wanadaiwa na kwamba serikali
inafanya uhakiki wa madai hayo kabla ya kuanza kulipa.
Alisema
kumekuwa na udanganyifu katika kuorodhesha madeni ya wazabuni hao kwa
kuweka fedha nyingi ambazo siyo za kweli na ndiyo maana serikali imeamua
kuhakiki kabla ya kulipa na mara zoezi hilo litakapomalizika watalipwa.
Shule
za sekondari zilifungwa Machi 28, hadi Aprili 12, mwaka huu, kwa ajili
ya mapumziko na shule nyingi zilifunguliwa kati ya Aprili 08 na 12,
mwaka huu.
Aidha,
kutokana na uhaba wa chakula katika baadhi ya shule waliongeza siku za
likizo na kuna shule ambazo hazijafunguliwa hadi sasa.
Shule
hizo zilizopo katika mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro, Kagera, Dodoma,
Tabora, Mtwara na Lindi, baadhi ya wanafunzi walieleza kuwa baada ya
kufika shule walitangaziwa kuwa hakuna chakula, hivyo wanaotakiwa kubaki
ni wanaotakiwa kufanya mitihani ya Taifa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.