Mchaka Zaidi

Thursday, April 30, 2015

Yanga kuibeba Simba CAF?


BAADA ya watani zao wa jadi Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu vita ya kuwania kushiriki michuano ya kimataifa sasa mwakani imesalia kwa vigogo wengine wa soka nchini Simba SC na Azam FC.

Yanga SC kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, huku wakiziachia kivumbi Simba na Azam ambazo mechi zao za mwisho katika Ligi Kuu ndizo zitaamua nani atatwaa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa namna hali ya mambo ilivyo, Simba ili kupata tiketi hiyo inalazimika kukesha usiku na mchana kuomba dua wapinzani wao Azam wapoteze mechi zao za mwisho ili kupata tiketi hiyo ambayo wanaisotea kwa miaka mitatu bila mafanikio.

Simba ipo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 41 nyuma ya Azam waliopo nafasi ya pili wakiwa na pointi 45, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi wanapanga kuwafanyia kitu mbaya Wanalambalamba hao katika mchezo utakaozikutanisha timu hizo Jumamosi wiki hii.

Iwapo Azam itashinda dhidi ya Simba ni wazi wekundu hao wa Msimbazi wamepoteza tiketi ya CAF kwa msimu wa nne, kwani hawataweza kuzifikia pointi za Wanalambalamba.

Itakumbukwa Azam licha ya kuizidi Simba kwa pointi nne pia ina faida ya mchezo mmoja mkononi.

Kama Simba watashinda mchezo huo itabidi waungane na mashabiki wa Yanga kuwashangilia mabingwa hao wapya watakapocheza na Azam FC, ili kuzidi kutanua wigo wa kufukuzia nafasi ya pili hali inayofanya vita ya kuwania tiketi ya CAF kuwa na uhondo wa aina yake.

Simba wamebakiwa na michezo miwili dhidi ya Azam FC na JKT Ruvu, huku Azam wakibakiwa na michezo mitatu dhidi ya Yanga na Mgambo JKT Ruvu.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.