Mchaka Zaidi

Wednesday, April 22, 2015

Mambo Yameiva: Mmiliki wa Gombe high School, Dkt Yared Fubusa Atangaza Nia Ya Kugombea Ubunge Jimbo La ZITTO KABWE Kwa Tiketi ya CHADEMA


Mwanzilishi na  Mkurugenzi wa Gombe school of Environment and Society (GOSESO) na mmiliki wa Gombe high school, Dkt Yared Fubusa ambaye pia ni kada wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ametangaza nia ya kugomba ubunge jimbo la Kigoma kaskazini kupitia chama hicho.

Akiongea na mtandao huu, Dkt Fubusa amesema kuwa ameamua kutangaza nia ya kugombea ubunge na kipaumbele cha awali ni kuboresha Elimu,huduma za afya,miundombinu.

Amesema vipaumbe vyake baada ya kuchaguliwa pia ni pamoja na zahanati ya Bitale kuwa na hadhi ya hospitali ya wilaya,ujenzi wa sekondari katika  kata 14 , ujenzi wa soko   katika mji mdogo wa Mwandiga ikiwa ni sambamba  na ujenzi wa viwanda  vya uchakataji wa juisi ya matunda matunda,kahawa na mchikichi ili kuongeza thamani ya bidhaa na kupunguza kero ya ajira kwa wananchi wa jimbo hilo.

Amesema endapo wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini watampa ridhaa ya kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atajitahidi kutengeneza fursa za ajira hasa za makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana na akina mama kwa kuishawishi Serikali itakayokuwepo madarakani,kuhakikisha inaleta wawekezaji mbali mbali jimboni.

Amesema ahadi hizo si za kubahatisha kwa kuwa anawafadhili na marafiki zake  kutoka marekani ambao wapo tayari kumuunga mkono ili kuleta maendeleo katika jimbo la Kigoma Kaskazini,pia amesema  wakazi wa vijiji vilivoporwa ardhi na hifadhi ya Gombe mwaka 1968 watafidiwa  haki zao ambazo waliondolewa bila kufidiwa.

Ameongeza kwa kusema pia katika jimbo hilo kuna changamoto ya kuongezeka kwa  chanzo cha mapato katika mwalo wa kijiji cha Kalalangabo kwa kujengwa  forodha ili kuongeza mapato kwa halmashauri akiwa Mbunge atashughulikia hilo swala pia.

''Rais Jakaya Mrisho Kikwete ni kiongozi anayeunga mkono uthubutu wangu kwani mimi ni  kijana pekee mzalendo ,jasiri na mwenye uchungu wa kuwaondoa watu wa jimbo la Kigoma kaskazini  katika janga la umaskini kwa kuwa ametoa ajira zaidi ya watu 50 katika shule ya  sekondari Gombe na timu ya Mvuvumwa” amesema Mgombea huyo mwenye Phd ya uchumi,maliasili na mazingira.

Dk.Fubusa amesema kwamba wananchi wanapaswa kutathimini uwajibikaji wa mgombea katika jimbo husika kwa kigezo cha mahusiano bora yenye maslahi kwa jamii hiyo ,ili kuepuka viongozi wanaokimbilia kuishi mijini baada ya kupata ubunge  na kuwataka wananchi wasikubali kuchagua viongozi wa aina hiyo ambao wapo kwa  maslahi binafsi.

Dk Fubusa ni mzaliwa katika kijiji cha Kiganza Kata ya Mwandiga Mkoani Kigoma.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.