Mchaka Zaidi

Tuesday, April 14, 2015

JWTZ iliandaa mabasi 300 kuukabili mgomo wa madereva


Kutokana na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria nchi nzima uliofanyika Ijumaa iliyopita, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilikuwa limeshaandaa mabasi 300 ambayo yangetumika kusafirisha abiria, imebainika.
 
Chanzo cha habari kutoka serikalini kimebainisha kuwa JWTZ ilikuwa imeweka tayari mabasi hayo na kuwa walikuwa wakisubiri taratibu za kufanya kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kujua safari za mabasi hayo na nauli ambayo wangewatoza wananchi.
 
Taarifa za ndani zinabainisha kuwa mgomo wa madereva wa abiria ulipangwa kufanyika kwa zaidi ya siku mbili, jambo ambalo lilifanya serikali kuliandaa jeshi kuwa tayari kutoa huduma kwa wananchi.
 
Ijumaa iliyopita, mamia ya abiria katika maeneo mengi ya nchi walipata madhila na mahangaiko baada ya madereva wa mabasi ya abiria nchi nzima kugoma, wakishinikiza serikali kubadili masharti ya kutakiwa kusoma kila wanaposajili leseni zao za udereva kila baada ya miaka mitatu, na matumizi ya tochi barabarani unaofanywa na askari wa usalama barabarani.
 
“Mbali na kulinda mipaka ya nchi kutoka kwa maadui wa nje, jeshi pia lina wajibu wa kuimarisha amani na usalama, na pia kufanya shughuli za kijamii kama vile kuingilia na kutoa huduma fulani muda wowote wanapotakiwa kufanya hivyo na serikali,” ilibainika.
 
Huu ni ushahidi kwani JWTZ imekuwa ikishiriki kusaidia jamii katika masuala mbalimbali wanapohitajika, ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vyao kujenga madaraja ya dharura, kuokoa maisha ya watu na kutolea mfano wa mafuriko ya Jangwani mwaka 2011 ambapo Jeshi lilishiriki katika kuwaokoa watu waliokuwa wamekwamba kwenye nyumba zilizokuwa zimezingirwa na maji.
 
Chanzo cha habari kimebainisha kuwa Jeshi lina mabasi mengi, na kutoa mfano tukio la hivi karibuni nchini Malawi wakati Rais Peter Mutharika alipotangaza hali ya hatari, JWTZ ilitoa malori 46 yaliyotumika kusafirisha msaada wa mahindi na dawa kwenda Malawi.
 
Kwa mujibu wa Nyasa Times, Serikali ya Tanzania ilichangia tani 1,200 za mahindi na dawa za binadamu katika kuisaidia serikali ya Malawi kupunguza uhaba wa chakula na magonjwa miongoni mwa maelfu ya Wamalawi kutokana na mafuriko ambayo yaliikumba nchi hiyo. Msaada huo ulikabidhiwa kwa Malawi na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Patrick Tsere.
 
Mgomo wa maderva wa mabasi ya abiria ya mikoani na baadhi ya mabasi ya Usafiri Dar es Salaam maarufu kama daladala uliibua vurugu katika kituo cha mabasi ya kwenda mikoani, hali iliyolazimisha askari Polisi kutumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya amani.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.