Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kutafakari jinsi kitakavyompata mgombea wake atakayepeperusha bendera ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,
Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho mkoa wa Arusha, Yona Merisho Nnko (74), ametoa ya moyoni akisema adhabu iliyotolewa na chama chao kwa makada sita kwa madai ya kuanza mapema kampeni za urais, inamlenga zaidi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Nnko
akizungumza na wanahabari nyumbani kwake kijiji cha Kikatiti, wilayani
Arumeru, mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema makada wote waliopewa
adhabu na chama hicho anawafahamu, lakini anayemfahamu zaidi ni Lowassa
ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kwamba amelegwa zaidi katika adhabu
hiyo.
“Lowassa
amehisiwa tu kwamba huenda kutokana na uchapaji kazi, uaminifu na
uhodari wake wa kuchukua hatua na maamuzi magumu, basi imekuwa nongwa
kwa baadhi ya watu wenye chuki ndani ya chama kumzushia mambo bila
ushahidi,” alisema.
Alisema
wakiwa na Lowassa mwaka 2005 walihangaika sana bila kulala ili
kuhakikisha mgombea wa CCM wakati huo, Rais Jakaya Kikwete, anashinda
kiti cha urais, na ikawa hivyo.
Alisema hata Rais Kikwete mwenyewe katika nafsi na moyo wake anatambua hilo hata akiamshwa usiku wa manane na kuulizwa.
“Namshauri amuunge mkono ndugu yake lakini asimpendelee,” alisema Nnko ambaye kwa sasa anajishughulisha na kilimo.
Aliwaomba Watanzania wakati ukifika kuhakikisha wanachagua kiongozi atakayejali maslahi yao na ya nchi kwa ujumla.
Alidai
kuwa ndani ya chama hicho kwa sasa hakuna anayemfikia Lowassa kwani
anajali makundi yote ya wananchi yakiwamo ya vijana, akina mama,wazee na
watoto.
“Lowassa
amefanya mengi kwa nchi yetu, naomba Watanzania muda ukifika tumchague
kuwa Rais wetu na mimi namshauri asiogope muda ukifika achukue fomu
agombee kwani wananchi wako nyuma yake,” alieleza.
Hata hivyo, alisema CCM inayo hazina kubwa ya wagombea ambao wanaweza kufaa kwa nafasi yo yote ya uongozi.
Katika
hatua nyingine, Nnko alitoa angalizo kuhusu tabia ya kila mmoja ndani
ya chama hicho kupayuka na kujifanya ‘msemaji’ wa chama.
Alisema
tabia hiyo inakidhoofisha chama huku wanachama wakikosa mweleko,
wasijue nani wamsikilize, hali inayotishia kukisambaratisha kabisa
chama ikiwa hali hiyo haitadhibitiwa.
Alisema
viongozi wa chama wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuwa na msemaji mmoja
badala ya sasa ambapo kila mmoja amekuwa msemaji jambo ambalo
linasababisha chama na wanachama kukosa mwelekeo.
Nnko
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Arusha kwa kipindi cha miaka
14 mfululizo kuanzia 1993 hadi 2007, alisema vurugu, makundi ndani ya
chama pamoja na chuki miongoni mwa baadhi ya viongozi na wanachama
yanatishia kukisambaratisha chama hicho.
Alisema
kitendo cha baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kukurupuka na
kutoa matamko aliyoyaita ya kupayuka ovyo, huku wakitoa vitisho kwa
baadhi ya wanachama bila kufuata vikao halali ni kujitafutia umaarufu na
kudhoofisha chama.
Alisema
zamani wakati chama kikiwa imara na chenye nidhamu, msemaji wa chama
alikuwa mwenyekiti au kama sio yeye basi atatoa kibali maalum kwa katibu
mkuu wa chama na matamshi yote ya chama yanatokana na vikao sio
kupayuka tu.
Alisema
akiwa kama mwenyekiti mstaafu anaamini Rais Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM ni kiongozi madhubuti, lakini baadhi ya viongozi wa
juu ndani ya chama wanataka wawe maarufu kuliko mwenyekiti kwa kupayuka
ovyo nje ya vikao.
Alisema
CCM kwa wakati huu kinakabiliwa na upinzani mkubwa hali ambayo
inakifanya kuwa dhaifu katika maeneo maeneo mengi hususani ya kuisimamia
serikali ili viongozi wake wafuate sheria, kanuni na maadili.
Februari
mwaka jana, Kamati Kuu (CC) ya CCM ilitangaza adhabu dhidi ya makada
wake sita kwa kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho
kwa miezi 12, huku pia wakiwa chini ya uangalizi.
Mbali
na Lowassa, wengine waliokumbwa na adhabu hiyo baada ya kuitwa na
kujojiwa mjini Dodoma ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja.
Makada
hao walipewa adhabu hiyo baada ya kuitwa na Kamati Ndogo ya Nidhamu
chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, na
kuwahoji kwa tuhuma za kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao kabla ya
wakati.
Adhabu
dhidi ya makada hao ilimalizika Februari mwaka huu, lakini
haijatenguliwa na vikao vya juu vya chama hali inayotia mashaka
kuhusiana na hatma yao.
Baadhi yao wamekwishatangaza nia ya kuingia katika kinyang’anyiro cha urais mwaka huu.
Makada wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka huu ni pamoja na Lowassa, Sumaye, Membe na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Wengine
ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi; Ngeleja; Spika wa
Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro;
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark Mwandosya na
Wasira.
Hadi
sasa makada wa CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania urais kupitia
chama hicho ni pamoja na Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu Mizengo
Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.