CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wadau wa habari
na taasisi mbalimbali, zikiwemo za kimataifa kuangalia kwa makini na
kujadili baadhi ya vifungu vilivyopo katika muswada wa habari ili
kuishawishi serikali kutousaini kwa kuwa unalenga kubana uhuru wa vyombo
vya habari nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika,
alisema miswada yote ya hati ya dharura, hasa ya miamala ya
kielektroniki na mitandao ya jamii isisainiwe ili iweze kurudiwa
bungeni.
“Wadau na taasisi mbalimbali za kimataifa wazipime ili waone kama
zinafaa, wakati hayo yakiendelea tunamtaka Rais Kikwete asisaini sheria
hizi, hasa ile ya makosa ya mitandaoni,” alisema Mnyika.
Alisema miswada yote iliyopelekwa kwa hati ya dharura inapaswa irudishwe
tena bungeni ili iweze kujadiliwa na wabunge kwa kushirikiana na wadau
wa habari.
Kwa mujibu wa Mnyika, kwakuwa miswada hiyo haijapelekwa kwa hati ya
dhati, hivyo wananchi wanapaswa kuibua mijadala ili kuhoji upungufu
wake.
Alisema endapo muswada wa habari utapitishwa kutakuwa na utaratibu wa
kuwa na Bodi ya Ithibati ambayo inataka kila mwandishi awe na elimu ya
shahada, hali itakayosababisha waandishi wengi kupoteza kazi.
Akizungumzia muswada wa takwimu, alisema serikali ina mpango wa kutoa
madaraka makubwa kwa Ofisi ya Takwimu (NBS) pamoja na kuzuia mikataba ya
gesi na mengineyo kupitia sheria hiyo.
“Haki ya kupata taarifa imetolewa sehemu moja, hili ni kosa na wana
lengo la kutumia sheria hizo mbovu kuwaadhibu wanahabari,” alisema
Mnyika.
Alisema endapo Rais akisaini muswada wa sheria ya kielektroniki, atakuwa
amefanya kosa kwa sababu wakati unapitishwa bungeni akidi ilikuwa
haijatimia.
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.