Mchaka Zaidi

Saturday, April 25, 2015

CCM Wamjibu Dr. Slaa Kuhusu NEC......Wakanusha Kukisaidia Chama Kipya Cha ACT-Wazalendo



Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amekanusha madai yaliyotolewa na  Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika ngome za CCM na kueleza kuwa  huo ni upotoshaji mkubwa kwani Tanzania  nzima ni ngome ya chama hicho.


Mbali na hilo amekanusha pia tuhuma zilizotolewa kuwa chama hicho kinakisaidia Chama cha ACT Wazalendo, akisema hawana sababu ya kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Nape alisema ratiba ya NEC haijapangwa kimkakati kama alivyodai Dk. Slaa kwani kila Mtanzania ataandikishwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kauli hiyo ina lengo la  kuwapotosha na kuwapa hofu wananchi.

"Kwa kauli hizi ni uthibitisho tosha kuwa  wenzetu vyama vya upinzani hasa Chadema siasa zao zina lengo la kuwagawa watu kikanda, uthibitisho wa mbegu mbaya ya chuki,"  alisema na kuongeza:

"CCM wanalaani vikali siasa za namna hiyo kwani  siyo hoja za msingi ila ni za kuwagawa wananchi na kupandikiza chuki zisizokuwa na maana na suala hilo linaonyesha jinsi wapinzani wanavyofanya siasa za kikanda."

Nape alisema wapinzani wanajua kuwa watashindwa na CCM ndiyo maana wanafanya fitina na kuwataka kuwagawa wananchi.
 
Alivitaka vyama vya siasa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha badala ya kueneza upotoshaji na kuwatia hofu zisizo na msingi kwa wananchi.

Akizungumzia kuhusu ACT Wazalendo, Nape alisema CCM haina  sababu ya kusaidia chama kingine cha siasa hivyo uvumi huo ni uchafuzi wa kisiasa.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.