Mchaka Zaidi

Tuesday, April 14, 2015

Nape awajibu wanaoishinikiza CCM... kuhusu ratiba ya uchaguzi




 
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema chama hicho hakitaendeshwa kwa mashinikizo ya watu wanaotaka kitangaze haraka ratiba ya uteuzi wa wagombea wake kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao. 
 
Kauli ya Nape imekuja baada ya baadhi ya makada wa chama hicho kuhoji inakuwaje CCM kinachelewa kutoa ratiba ya mchakato wa uchaguzi, wakati muda unasonga.
 
Aprili 6 mwaka huu, akaunti ya mtandao wa Twitter iliyosajiliwa kwa jina la Waziri wa Zamani wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Hamis Kagasheki, ulihoji “CCM ni chama cha wanachama wote. Hii ni Aprili hakuna ratiba au utaratibu wa wanachama kumpata mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama. Kulikoni?”
 
Kagasheki mwenyewe hakupatikana kuzungumzia ujumbe huo, baada ya simu yake ya mkononi kuuita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe wa simu hakujibu.
 
Mbali na Kagasheki, makada kadhaa wa chama hicho pia wamekuwa wakihoji mantiki ya chama hicho kuzuia watu wasitangaze nia kabla ya wakati.
 
Majibu ya Nape
Nape alisema vikao vya chama ndivyo vitakavyoamua mchakato huo uanze lini, lakini CCM haina historia ya kuwahi wala kuchelewa. 
 
“CCM mara nyingi huandaa ratiba yake kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec). Hao wanaotaka kuharakisha mambo wajaribu kupitia mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010, CCM ilitangaza uteuzi muda gani. Kwanini safari hii wanatia presha?” alihoji.
 
Mapema mwezi uliopita Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipokuwa alipozungumza na wajumbe wa halmashauri ya Jimbo la Same Magharibi wakati akishiriki na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, alisema uteuzi wa wagombea wa udiwani, ubunge na Urais utafanyika Juni.
 
Lakini Nape juzi alisema hata hiyo Juni iliyotangazwa awali na Kinana haijapitishwa na chama, hivyo bado tarehe rasmi ya uteuzi haijatolewa.
 
Mwaka 2010, ratiba ya uteuzi wa wagombea katika chama hicho tawala ilitangazwa mwanzoni mwa Juni na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.