Watu 10 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja anayesadikiwa kuhusiana na watu hao
waliokamatwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kumjeruhi kwa
panga askari polisi aliyekuwa akipambana naye.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa polisi mkoani
Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo lilitokea juzi (Aprili 14
mwaka huu) majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha Nyandero,
tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.
Kamanda Paul alimtaja mtu aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo ambaye umri
wake haujafahamika ambaye ni mkazi Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha alisema siku ya tukio polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema
kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa kuwa wanajihusisha na matukio
mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua kufatilia nyendo zao.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema: “Polisi walipata taarifa
kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili kwenda kusikojulikana na
wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia ndipo walikutana na bajaji
moja ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo na kuisimamisha.”
Alisema kuwa bajaji hiyo iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza
kukimbia ndipo askari mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza
kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia alilokuwa
nalo na kumkata askari huyo eneo la shingoni.
Askari mwingine mwenye namba E.9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma
alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa huyo,ambapo alipoanguka
chini wananchi wa eneo hilo tayari walifika katika eneo hilo na kuanza
kumshambulia marehemu huyo kisha kumchoma moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti huo
kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao
wanatiliwa mashaka,”Alisema kamanda Paul
Alisema polisi waliendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.