Mchaka Zaidi

Thursday, June 18, 2015

Godbless Lema Nusura apigane na Polisi kituo cha Uandikishaji


MBUNGE wa   Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) jana nusura apigane  na askari aliyekuwa akilinda   kituo cha kujiandikisha katika  daftari la wapiga kura cha Shule ya Msingi Mkombozi Kata ya Sokoni I.

Tafrani hiyo ilitokea    saa 5.00 asubuhi wakati Mbunge huyo
alipokuwa akitembelea vituo vya kujiandikisha kupiga kura  jijini Arusha   akifuatana na waandishi wa habari. Uandikishaji huo ulianza juzi.

Lema alipofika kituoni hapo alikuta foleni kubwa nje ya lango la kuingia kituoni hapo huku ndani ya lango hilo akiwamo askari wa kike aliyekuwa amevalia kiraia.

Askari huo  alikuwa akiandikisha majina ya wananchi hao na kuwataka waondoke  hadi kesho yake  kupata vitambulisho.

Kutokana na hali hiyo Lema alibishana na askari huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana na kumnyang’anya kalamu aliyokuwa akitumia kuandika majina hayo katika daftari dogo huku akiwaambia polisi hao wanavunja sheria.

Majibizano kati ya Lema na askari huyo wa kike yalisababisha askari mwingine wa kiume  kuingilia kati na baada ya mabishano makali na Lema, walishikana wakitaka  kupigana kabla ya kuamriwa na viongozi waliokuwa wamefuatana na Lema.

“Haiwezekani polisi akaandikisha majina na kuwaambia watu waje siku inayofuata  waweze kufanya taratibu za kupewa vitambulisho.

”Polisi wajibu wako hapa kituoni ni kuangalia usalama na siyo vinginevyo, utaratibu mnaoufanya ni kosa.  Hata mawakala wa vyama vya siasa waliopo hapa hawana majina haya.

“Tutajuaje mnaenda kuyabadilisha au kuuza hili daftari na kutuletea majina mengine ... na daftari hili    halina muhuri wa aina yoyote,” alisema Lema.

Tafrani hiyo ilisababisha Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha (OCS),Thomas Mareko kufika  kituoni hapo  naye akaendelea kubishana na Lema aliyesisitza kuwa polisi walikuwa wanafanya makosa.

Hatimaye mmoja wa wawakilishi wa Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Jiji la Arusha alifika kituoni  hapo na kuzungumza na Mbunge huyo pamoja na OCS pembeni.
Chanzo: Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.