HARAKATI za kuwania ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini zimeanza baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Abdulla Panju, kutangaza rasmi nia ya kugombea nafasi hiyo akiwa na kauli mbiu ya chagua maendeleo, usichague soda.
Panju alitangaza rasmi nia hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini hapa, ambapo aliwataka wanachama wa CCM kumuamini na kumpa nafasi ili apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aidha, alisema ameamua kujitokeza na hana mashaka yoyote kwamba yeye ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa kumng’oa mbunge wa sasa wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) kutokana na sifa adhimu pamoja na uzoefu wa uongozi alionao ndani na nje ya siasa kwa muda mrefu.
“Ninajiamini nina uwezo wa kulikomboa jimbo, ni haki yangu kama raia wa Tanzania na uongozi wangu utakuwa shirikishi. Tukishirikiana wananchi ninaamini tutasukuma mbele gurudumu la maendeleo la wananchi wa Arusha.”
Aliwaasa wanachama na wagombea wa chama hicho kuungana na kujenga undugu, upendo, urafiki na mshikamano ili kuepuka kujenga makundi mabaya ndani ya chama kwa misingi ya udini, ukabila na rangi.
Kada huyo wa CCM na ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Bushbuck Safaris ya jijini hapa, alitumia muda huo pia kuwaasa wananchi wa Arusha kuepuka siasa za vurugu na ugomvi ambazo alisema hazina tija kwao lakini pia tabia ya wagombea kuchafuana.
Chanzo: Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.