Mchaka Zaidi

Saturday, June 6, 2015

CCM Yawabana Wagombea Urais.....Yawazuia Kushiriki Midahalo, Kubandika Picha Magari Yao wala Kufanya Kampeni


WAKATI Watanzania na hasa viongozi wa sekta binafsi, wakijiandaa kupima uwezo na uelewa wa watangaza nia wa CCM, katika masuala muhimu ya kiuchumi kwenye mdahalo ulioandaliwa kesho kutwa, chama hicho kimepiga marufuku watangaza nia hao kushiriki midahalo hiyo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho mjini hapa jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, amesema chama hicho hakiruhusu midahalo kwa makada wake hao kwa kuwa hakina mgombea mpaka sasa.
 
“Nasikia kuna midahalo lakini CCM hairuhusu wanaotaka urais kushiriki kwa sababu hadi sasa wao ni wagombea tu,” alisema Dk Khatib.
 
“Kushiriki midahalo sasa ni kuchanganya wanachama, kulumbana na kupakana matope. Wagombea hao waache kushiriki midahalo.
 
“Na hao wanaoandaa midahalo wawasiliane na Makao Makuu kwa sababu kwa sasa hatuna muda mrefu, zimebaki wiki nne tu kwa ajili ya Mkutano Mkuu,” alisema.
 
Maandalizi
Kabla ya tamko hilo la CCM, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya CEO Round Table Tanzania (CEOrt), Ali Mufuruki alitangaza jana asubuhi kuwa mdahalo huo umeandaliwa na tayari baadhi ya watangaza nia wameshathibitisha kushiriki.
 
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watangaza nia waliokuwa wamethibitisha kushiriki ni watano na mdahalo huo ulikuwa ufanyike mara tatu, mara ya pili ukihusisha watangaza nia wa vyama vya upinzani na mara ya tatu watangaza nia wengine kutoka CCM.
 
Watangaza nia hao ambao kutokana na tamko la Dk Khatib wamezuiwa kuonesha uwezo wao kwa Watanzania, ni aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye na mmoja wa wanadiplomasia wakubwa, Balozi Amina Salum Ali ambaye ni mwanamke pekee hadi sasa aliyejitokeza kutangaza nia na kuchukua fomu ya kugombea urais.
 
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
 
Mufuruki alisema, mbali na uthibitisho kutolewa na watangaza nia hao, lakini washiriki kutoka sekta binafsi waliotakiwa kulipia Sh 100,000 ya kiingilio, walishaanza kulipia na akahadharisha kuwa ambao wangechelewa huenda wasingepata nafasi, kwa kuwa ukumbi wa mjadala unachukua watu wasiozidi 300.
 
Mdahalo huo ulitarajiwa kurushwa moja kwa moja na televisheni mbalimbali nchini kwa saa mbili kuanzi saa mbili asubuhi siku ya Jumatatu ijayo, ambapo wagombea walikuwa waulizwe maswali na jopo la wataalamu wa uchumi na masuala ya utawala bora.
 
Maeneo waliyotakiwa kuzungumzia ambayo pia maswali yangetoka huko, ni pamoja na kipaumbele chao cha uchumi katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka 2020.
 
Pili wanatarajiwa kuzungumzia mikakati yao katika jitihada za kuhakikisha kunakuwepo utawala bora na kushinda vita dhidi ya rushwa.
 
Tatu, walitarajiwa wazungumze kuhusu malengo yao ya muda mrefu yatakayoleta maendeleo na kutunza utajiri wa maliasili wa Tanzania.
 
Pia walitarajiwa watoe maoni yao kuhusu dira zao, mikakati na jitihada za kuipeleka Tanzania katika mambo muhimu yatakayoharakisha uchumi wa muda mrefu.
 
Hata  hivyo, Dk Khatib alisema kuruhusu wanachama hao kushiriki midahalo sasa ni kuruhusu malumbano, kuvuruga wanachama wenzao na kutukanana.
 
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa sasa CCM haina mgombea wa urais, hivyo haitakuwa vyema kwa wanachama hao wanaoomba uteuzi kuanza kushiriki midahalo.
 
Kampeni marufuku
Aidha, alisisitiza kauli yake ya juzi kuwa wanaochukua fomu wanatakiwa kwenda kusaka wadhamini mikoani na siyo kuendesha kampeni au kuomba kura.
 
“Wanakwenda kuomba wadhamini siyo kampeni. Kampeni hazijaanza, wajihadhari na hilo kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha kanuni na taratibu za chama,” alionya.
 
Alisema huu si muda wa kwenda na mabango na picha katika kusaka wadhamini, kwani mikoa na wilaya imeelekezwa kutenga eneo maalumu tu kwa ajili ya waliochukua fomu kudhaminiwa na wenzao.
 
“Mabango na picha pia haziruhusiwi, huu sio muda wa kampeni. Na hakuna mgombea hata mmoja atakayekosa mdhamini,” alisema Katibu huyo wa Oganaizesheni.
 
Chanzo: Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.