Mchaka Zaidi

Sunday, May 3, 2015

Vurugu Burundi: Wakimbizi 800 Waingia Nchini

 
WAKIMBIZI 800 kutoka nchini Burundi wameingia nchini kupitia mkoani Kigoma huku wengine 87 wakirejeshwa nchini mwao baada ya kuingia nchini kwa kupitia wilayani Ngara mkoani Kagera.
 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Isack Nantanga alisema wakimbizi hao wameingia nchini kwa makundi madogo madogo na watahifadhiwa kwa muda katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
 
Akizungumza na mtandao  huu jana,Nantanga alisema wakimbizi wanaofikia 800 wameshaingia nchini huku walioingia kupitia mkoani Kagera ilibidi warejeshwe walipotoka kutokana na kukiuka sheria za kimataifa kwa wakimbizi kuingia nchi nyingine wakivuka nchi moja.
 
Walianzia Rwanda.
Alisema hawapokei wakimbizi wanaotokea Rwanda kutokana na kuwa sheria za kimataifa haziruhusu wakimbizi kuvuka nchi moja ndiyo maana waliwarejesha wakimbizi hao. 
 
Alisema kati ya wakimbizi hao waliopokelewa mkoani Kigoma wameingia kupitia vijijini ambapo serikali za vijiji wanawapokea na kuwahoji kisha kuwapeleka kigoma mjini kwenye kituo maalum.
 
Alisema serikali za vijiji na wilaya kwa kushirikiana na halmshauri wamekuwa wakaifanya kazi ya kuwahoji kujua sababu hasa ya kuwafanya wakimbilie nchini humu kwani isije kutumika vurugu za Burundi watu kuingia nchini.
 
“Serikali kwa kushirikiana na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) baada ya kuwahoji na kuwapa misaada muhimu wanaobainika kupata hifadhi wana mpango wa kuwapeleka kwenye kambi ya Nyarugusu kwa muda,”alisema.
 
Msemaji huyo alisema baada ya kuhifadhiwa katika kambi hiyo mipango inaendelea kufahamu njia nyingine za kuwahifadhi.
 
 Kutoka Kigoma 
Mratibu wa idara ya wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya ndani kanda ya Magharibi Kigoma,Tonny Laiser amesema kuwa wakimbizi hao wameanza kuingia mkoani Kigoma wakipitia maeneo tofauti ya mpaka kati ya mkoa huo na nchi ya Burundi.
 
Wengi wa wakimbizi hao wametokea mji wa Bujumbura na wameingia Kigoma kwa usafiri wa boti kupitia bandari ndogo ya Kibirizi mjini Kigoma.
 
Inaelezwa kuwa kundi kubwa la wakimbizi liliingia nchini juzi katika mpaka wa Tanzania na Burundi kwenye kijiji cha Kagunga mwambao wa kaskazini wa ziwa Tanganyika ambapo kundi la wakimbizi 200 waliingia kupitia kijiji hicho.
 
Tayari wakimbizi 68 ambao waliingia na kufikia kambi ya muda ya NMC kibirizi mjini Kigoma wamepelekwa kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu ambayo kwa sasa ndiyo kambi pekee mkoani Kigoma inayohifadhi wakimbizi.
 
Akizungumzia kuingia kwa wakimbizi mkoani humo Mkuu wa mkoa Kigoma, Issa Machibya alisema kuwa wameanza kupokea wakimbizi kutoka vijiji mbalimbali vya wilaya za Buhigwe,Kasulu na Kibondo ambao wanakimbia hali ya machafuko nchini Burundi.
 
Machibya alitaja maeneo ambayo hadi sasa yamekuwa yakipokea wakimbizi hao kuwa ni pamoja na Kijiji cha Kagunga wilaya ya Kigoma, Muyama,Kibande na Kilelema ambavyo vyote vipo katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
 
Kuingia kwa wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania kunatokana kuanza kwa machafuko nchini humo kati ya wananchi wanaopinga kitendo cha Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza kuongoza muhula wa tatu wa uongozi dhidi ya polisi na wanajeshi wanaomtii raisi huyo.
 
Kwa siku mbili mfululizo kumekuwepo na taarifa za kuchomwa mwa mabasi mawili ya abiria na moja kulipuliwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono huku kukiwa na vifo vya watu kadhaa kutokana na makabiliano ya waandamanaji na polisi.
 
Wageni wamekuwa wakizuiliwa kuingia mji mkuu wa Burundi, Bujumbura ambako kwa kiasi kikubwa maandamano ya kupinga hatua ya Rais Nkurunzinza kuongoza muhula wa tatu yanaendelea ambapo kwa sasa maandamano hayo yameanza kusambaa mikoa ya jirani na mji Mkuu wa Bujumbura.
 
Kwa upande wa wilaya ya Ngara, Mkuu wa wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu amesema Serikali ya Tanzania imewarejesha wakimbizi 87 waliotokea Burundi kwa madai kuwa wamekimbia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
 
Wamerejeshwa kutokana na kutofuata taratibu za kuomba hifadhi ya ukimbizi. Aliuambia  mtandao huu jana mjini Ngara kuwa kuanzia Aprili 29 mwaka huu mpaka Mei mosi waliingia wakimbizi 87 kutoka Burundi kupitia njia za panya bila kufuata utaratibu ambapo walipokamatwa na kuhojiwa walidai wanakimbia mapigano yanayoendelea nchini mwao.
 
“Tulipopata taarifa tuliwasaka na kuwakamata kisha tukawasiliana na Serikali yao ambapo walituhakikishia usalama wa watu wao na kutuomba tuwarejeshe nchini mwao kwa sababu hali ni shwari na sisi jana tuliwarejesha kwao ambapo walipokelewa na uongozi wa Serikali yao,”alisema Kanyasu.
 
Alisema baada ya kuwarejesha makwao hakuna taarifa nyingine za kuonekana wakimbizi wakiingia wilayani huo kwani wananchi kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama wanahakikisha kila anayejipenyeza wanamtambua na kutoa taarifa.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.