Mzazi mwenzake staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, Siwema Edson (27) ametiwa mbaroni na kusota rumande kwa siku kadhaa akidaiwa kujipatia mali kwa njia ya vitisho kutoka kwa kigogo mmoja serikalini (jina linahifadhiwa kwa sasa).
Mei 2, mwaka huu, Siwema alilala ‘nyuma ya nondo’ (mahabusu) kwa siku mbili katika Kituo Kikuu cha Polisi, Wilaya ya Nyamagana jijini hapa baada ya kukamatwa nyumbani kwake Lumala, Manispaa ya Ilemela.
Kwa mujibu wa chanzo, awali ilidaiwa kuwa, Siwema aliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na kigogo huyo jijini hapa kwa ahadi ya kufunga naye pingu za maisha kufuatia kigogo huyo kufiwa na mkewe.
Ikazidi kusemekana kwamba, wawili hao wakiwa ndani ya uhusiano, Siwema hakuwahi kumfahamisha kuwa ana mchumba ambaye ni Nay. Ikafika mahali, kigogo akamvisha pete ya uchumba, picha zikatoka kwenye gazeti moja .
Ilizidi kuelezwa kuwa Nay baada ya kugundua kuwa Siwema amevishwa pete ya uchumba na kigogo huyo, alihamanika kiasi kwamba taarifa zilimfikia kigogo huyo wa serikali naye akaamua kujitoa kwa Siwema, akaoa mwanamke mwingine.
“Tatizo Siwema hakuwa muwazi kwa kigogo kwamba, Nay ni mchumba wake. Lakini kabla ya kigogo kumtema Siwema, kumbe alishawahi kumpiga picha za utupu mwenyewe akiwa hajui.”
“Sasa baada ya Siwema kumwagwa kutokana na kelele za Nay kwamba demu ni mchumba wake, ndipo zile picha Siwema alizitumia kumtishia amnunulie gari vinginevyo angemwanika kwa kuzitupia kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook,” kilieleza chanzo hicho.
Ikazidi kuelezwa kuwa, aliposikia vitisho hivyo, kigogo huyo aliamua kumweleza mkewe juu ya sakata zima ambapo walikubaliana kumnunulia Siwema gari na akampa na kiasi cha fedha kwa masharti ya kuzifuta picha hizo kutoka kwenye simu yake.
“Lakini Siwema licha ya kununuliwa gari aina ya Honda CRV na akapewa na kiasi cha fedha alichotaka, bado hakuzifuta picha hizo kwenye simu yake.
“Kana kwamba haitoshi, aliendelea kumtishia tena ambapo safari hii alitaka atumiwe kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mtaji wa biashara, jambo lilimnyong’onyeza kigogo huyo na kuamua kwenda kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola kwa hatua za kisheria,” kilisema chanzo.
Akizungumza na gazeti la Ijumaa Wikienda mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi, Charles Mkumbo alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Alisema Siwema alikamatwa baada ya mlalamikaji kutoa taarifa kwa jeshi hilo ambapo walifungua jalada la uchunguzi Mei 2, mwaka huu na siku hiyohiyo walimkamata mtuhumiwa akiwa nyumbani kwake, Lumala Manispaa ya Ilemela.
“Ni kweli tulimkamata Siwema Edson (27), mkazi wa Lumala. Ametuhumiwa kujipatia mali kwa njia ya vitisho. Awali alikuja mlalamikaji kabla ya kukamatwa.
“Hawa watu awali walikuwa wapenzi. Katika mapenzi yao, siku moja, Siwema alimpiga picha za utupu mlalamikaji bila yeye kujitambua wala ridhaa yake,” alisema DCP Mkumbo.
Alisema baadaye uhusiano wao ulivunjika, ndipo Siwema akatumia picha hizo kumtishia kuwa kama hatatimiza matakwa yake kwa kumnunulia gari na kumpa fedha, basi angezisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook.
“Mlalamikaji alitimiza matakwa ya mtuhumiwa kwa kumnunulia gari aina ya Honda CVR lenye namba za usajili T103 DDU na akamtumia na fedha. Lakini Siwema aliendelea kumtumia vitisho, akimtaka amtumie kiasi kikubwa cha fedha za mtaji, ndipo mlalamikaji akaja kutoa taarifa polisi, likafunguliwa jalada la uchunguzi na siku hiyohiyo akakamatwa,” alisema DCP Mkumbo.
Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa gari hilo linashikiliwa kituoni hapo huku Siwema akiachiwa kwa dhamana wakati upelelezi ukiendelea. Ukikamilika atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alisaini sheria ya makosa ya mtandao.
Sheria hiyo, inakataza mtu kutumia mitandao kwa nia ya kumchafua mtu au kuanika picha zake, hasa za utupu bila ridhaa yake.
Chanzo: Gpl/Ijumaa wikienda
Chanzo: Gpl/Ijumaa wikienda
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.