Mchaka Zaidi

Monday, May 4, 2015

MGOGORO: Kanisa la Moravian Wakataa Jimbo jipya.


KANISA la Moravian Jimbo la Mashariki limeitaka Serikali iangalie upya uamuzi wake wa kuruhusu mgawanyiko wa kanisa hilo kwa kuruhusu usajili wa Jimbo lingine ili kuepusha uvunjifu wa amani.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Jimbo la Mashariki,Dkt Clement Fumbo ambapo alisema endapo serikali itaruhusu hilo basi iruhusu na upande wao kusajili na kuendesha masuala yake  ili kuwa na amani.
 
“Tunaiomba serikali iwatahadharishe upande uliosajili Jimbo wasijihusishe na makanisa au shirika ambazo haziko upande wao kwa kutumia usajili walioupata vinginevyo watachukuliwa wamekwenda kuleta fujo”alisema Fumbo.

Aidha aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo inajua mgogoro uliopo kati ya pande mbili  tangu zamani kuwasiliana na pande zote ili kujua kinachoendelea kabla ya kusajili Jimbo jipya.
Clement alisema kuwa ni kwa muda mrefu Kanisa la Moravian jimbo la misheni ya Mashariki limekua na mgogoro ambao umeigusa jamii kutokana na machafuko ndani ya nyumba za ibada.
 
“Mgogoro huo umefikia mahali pa kuligawa kanisa hili katika makundi mawili huku kila kundi likiwa na Halmashauri yake iliopelekea kutokea kwa machafuko katika mashirika mbalimbali ikiwemo ushirika wa Kinondoni”alisema Fumbo.
 
Alisema tamko hilo ni kutokana na taarifa za  kusajiliwa kwa jimbo la upande wa pili huku ikisemekana uzinduzi wa Jimbo hilo jipya ukitegemewa kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
 
Mgogoro huo  ulipelekea kanisa la Moravian Duniani lenye Makao Makuu  nchini Norway kuingilia kati na kutaka kuondoa kesi inayowafanya walumbane mahakamani.
 
Hali hiyo ilitokea baada ya  kuondolewa nyadhifa na kusimamishwa kazi, Mwenyekiti wa Halmashauri Jimbo hilo, Clementi Fumbo na wenzake saba.
 
Fumbo na wenzake saba walifungua kesi ya madai namba 222 ya mwaka 2012, katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam wakipinga kuondolewa madaraka na kusimamishwa kazi.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.