PICHA YA MAKTABA.
Monduli. Mkazi mmoja wa Kijiji
cha Nanja, Kata ya Lepruko, wilayani Monduli, anadaiwa kumuuza mtoto
wake wa kumzaa kwa mtu mwingine kwa Sh70,000 kwa madai kuwa ana maisha
magumu.
Katika tukio
hilo la kushangaza, inadaiwa mwanamke huyo (jina linahifadhiwa) aliamua
kumuuza mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miezi minane katikati ya Mei,
mwaka huu akiwa ametoka naye mkoani Singida.
Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Nanja, Time Samsoni akizungumza juzi mbele ya Mratibu wa
Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (Tawla) Tawi la Arusha, Francisca
Gaspar alisema walijaribu kumshawishi akamchukue mtoto wake, lakini
aligoma.
Mwenyekiti Samsoni alidai kuwa mtu aliyemnunua
mtoto huyo anaishi katika Kijiji cha Longonito na ana wadhifa mkubwa
kijijini hapo.
“Kwa kweli tulisikitishwa na kitendo hicho
cha huyo mwanamke kumuuza mtoto wake kwa Sh 70,000 akisingizia maisha
magumu na ameshindwa kumlea,” alisema Samsoni.
Alisema
walimwita mwanamke huyo kwenye ofisi ya kitongoji na kumhoji sababu
zilizomfanya amuuze mwanaye, lakini aliwaaambia kuwa hana uwezo wa
kumhudumia.
Mratibu wa Tawla, Gaspar alisema watahakikisha
wanafuatilia suala hilo ili lipatiwe mwafaka. “Lakini tumeambiwa kuwa
mama huyo ametoroka baada ya kuhojiwa na viongozi wa hapa kijijini na
hajulikani aliko mpaka sasa.”
Alisema katika kipindi hiki
ambacho Tawla inaadhimisha miaka 25 tangu ianzishwe, wanatoa elimu ya
sheria kwa wanawake wa eneo la Nanja na Meserani, hivyo jamii iwe inatoa
taarifa kwao wanapoona matukio kama hayo.
Nina uhakika kuna
matukio mengi yanatokea huku vijijini ila taarifa zinashindwa
kufikishwa na endapo mngetuarifu mapema, tungeshirikiana na polisi huyo
mama aliyemuuza mtoto wake angekamatwa kabla ya kutoroka,” alisema
Gaspar.
Mkazi mmoja wa eneo hilo, James Lengitambi
alipongeza hatua ya mwanamke huyo kumuuza mtoto wake kuliko angemtupa
chooni au kwenye mfuko wa Rambo kama wanavyofanya wanawake wengine.
“Tumezoea
kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa baadhi ya wanawake wanawatupa
chooni watoto wao au kuwatelekeza kwenye mifuko ya plastiki, ila huyu
amemuuza hajamuua,” alisema Lengitambi.
Chanzo:
MWANANCHI
MTANDA BLOG
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.