MWANANCHI
Homa ya Uchaguzi Mkuu imeifanya Chadema kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu ili kujadili mambo ya kitaifa, ikiwamo adhabu waliyopewa wabunge wa Ukawa kabla ya kutoa tamko.
Kikao hicho kilichofanyika jana, pia kilihusisha wabunge walioadhibiwa kwa kufanya fujo bungeni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu ya mafuta na gesi kwa hati ya dharura na hivyo kupewa adhabu tofauti ya kutohudhuria vikao kuanzia viwili hadi vyote vilivyosalia.
Manaibu katibu mkuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) walisema kutokana na kuongezeka kwa homa ya uchaguzi, chama hicho kimelazimika kuitisha kikao hicho na kwenda tofauti na ratiba yake ya mwaka ili kuweka sawa baadhi ya mambo.
“Pamoja na ratiba iliyopo, kila litakapokuwa linajitokeza jambo muhimu tutakuwa tunaitana ili kulijadili kwa kina. Hali ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura Zanzibar ina ishara zote kuwa hatutakuwa na mwisho mzuri,” alisema Mwalimu na kufafanua kuwa kikao hicho kitakuja na jibu… “Kama hali hiyo haitarekebishwa, upo uwezekano wa athari zake kufika Bara pia.”
Mwishoni mwa wiki, polisi walifyatua risasi kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura baada ya wananchi kwenda eneo hilo kujaribu kuzuia kile walichokiita “wapigakura mamluki” na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa na baadhi yao kulazwa hospitalini.
Mwalimu alisema majibu rahisi yanayotolewa na Serikali kuhusu vurugu hizo kuwa zinafanywa na vikundi vya wahuni, yanatia shaka hasa kwa kuzingatia kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo na vinashuhudia mambo hayo yakitokea.
Alieleza kuwa matukio yasiyo ya kawaida hayatokei Zanzibar pekee, bali hata maeneo mengine, akitoa mfano kwenye uandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR ambako alisema kuna hali inayokanganya hivyo kufanya kuwapo umuhimu kwa chama kutoa tamko juu ya kinachoendelea.
“Wale walioandikishwa mwanzo kwenye wilaya za Mlele mkoani Katavi na Kilombero, Morogoro wameambiwa warudishe kadi walizopewa na waandikishwe upya. Hii siyo hali ya kawaida na hasa inafanywa katika majimbo ambayo ni ngome ya Chadema,” alisema na kuongeza:
“Pamoja na hayo yote, tutatangaza ushindi mapema sana wilayani Kilombero katika uchaguzi mkuu ujao.”
Kuhusu kikao hicho, Mnyika alisema kilijadili maandalizi ya jumla ya Uchaguzi Mkuu, kupokea taarifa za wagombea udiwani, ubunge na urais, taarifa ya majadiliano ya Ukawa pamoja na ile ya wabunge waliopewa adhabu.
Akitoa msimamo wa awali wa chama chake, Mnyika alisema wabunge hao walikuwa na sababu zote za msingi za kupinga miswada hiyo na kwamba taarifa zilizoripotiwa kuwa wanatumiwa hazina mashiko yoyote.
NIPASHE
Wapiga kura 11,248,198 kati ya milioni 22 waliotarajiwa kuandikishwa mwaka huu katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura nchini, wameshaandikishwa na sasa wanamiliki vitambulisho wakisubiri kuvitumia katika uchaguzi mkuu Oktoba, 25 mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ina uhakika wa kukamilisha uandikishaji kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) mapema mwezi ujao.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Danian Lubuva, alitoa kauli hiyo jana huko Msoga, Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani ambako Rais Kikwete alikuwa mmoja wa wananchi wa eneo hilo waliojitokeza kujiandikisha ikiwa ni siku ya kwanza kwa uandikishaji mkoani Pwani.
Jaji Lubuva alimueleza Rais Kikwete kuwa licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mchakato huo, hali ya uandikishaji ilipofikia nchini hadi Julai 06 inaendelea vema na matumaini ni makubwa kuwa uandikishaji ujao utakamilika mapema na kuwafikia walengwa wote waliokusudiwa.
“Mheshimiwa Rais, pamoja na changamoto nyingi na kelele nyingi zilizokuwa zikisikika huku na kule, tayari tumeandikisha watu 11,248,198 mpaka jana (juzi) kati ya lengo tulilojiwekea la kuwafikia watu kati ya milioni 21 mpaka 23, na mikoa iliyokuwa tayari imekamilisha ni 13, bado 11 ambayo nayo nakuhakikishia itakamilisha na mapema Agosti, kazi hii itakamilika,” Jaji Lubuva.
Baada ya kujiandikisha, Rais Kikwete aliipongeza Nec kwa hatua iliyofikiwa hadi sasa na kuwataka wasife moyo bali wachape kazi kikamifu ili uandikishaji ukamilike ndani ya muda na wananchi wawe na uhakika wa kupiga kura kwa kutumia vitambulisho hivyo.
Rais Kikwete alisema changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa zuandikishaji zichukuliwe kama fursa ya kukamilisha kwa wakati.
Rais Pia ametumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kujitokeza kujiandikisha ili watumie haki yao kumchagua kiongozi wanayemtaka kuanzia diwani, mbunge na rais na kwamba wasipofanya hivyo baadaye wasije kulalamikia viongozi watakokuwa madarakani ambao wamechaguliwa na wenzao waliojiandikisha.
NIPASHE
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa, amesema moja ya sababu inayochangia vurugu bungeni kwa sasa ni staili inayotumiwa na kiti cha Spika wa sasa, Anne Makinda, katika kuongoza mhimili huo.
Msekwa amesema kanuni zote za Bunge zipo vile vile tangu yeye alipokuwa madarakani na kwamba kilichobadilika kwa sasa ni aina ya wabunge waliopo.
Hata hivyo, hakufafanua kuhusiana na aina ya wabunge, lakini kwa sasa Bunge hilo lina idadi kubwa ya wabunge vijana pamoja na wabunge wengi kutoka upinzani.
Aliyasema hayo juzi usiku katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV na kituo cha redio cha Redio One.
Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, alisema kinacholeta mzozo ni namna kiti kinavyoongoza Bunge kwa maana ya staili inayotumika.
Aliongeza kuwa Bunge hilo lina mchanganyiko wa wabunge wa upinzani na CCM ambao pia wamo vijana wa kutosha na kwamba kiti hakiwezi kuendelea kutumia staili ile ile ya siku zote.
Msekwa ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee la CCM, alikiri kwamba siku za nyuma kiti cha Spika kilikuwa kinaheshimika tofauti na ilivyo sasa.
Mwanasiasa huyo alisema ni aibu na fedheha kwa wabunge kusimama na kuzomea huku Spika naye akiwa amesimama na kwamba jambo hilo halikuwapo wakati wa uongozi wake.
Alifafanua kuwa haya yanayotokea kwa sasa yanatokana na wakati huu kuwa ni wa kizazi kipya na kwamba ili kuongoza mhimili huo, ni lazima staili ibadilike.
Hata hivyo, Msekwa hakusema ni staili ya namna gani itakayoweza kulibadilisha Bunge na kuondoa mizozo ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara ikiwamo wabunge kutoka nje na kususia vikao.
NIPASHE
Wazee wanaolipwa pensheni na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanzia sasa watakuwa wakitumia kadi maalum kulipwa pensheni yao ya kila mwezi ili kuwalinda wasiibie fedha zao za mafao.
HABARILEO
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeiomba serikali kuu kulisuka upya jiji hilo kimuundo ili liwe na nguvu kisheria ya kutekeleza majukumu yake, kwa kuwa hivi sasa linashindwa kutokana na kuingilia mamlaka nyingine, hivyo linaonekana halifanyi kazi.
Hayo yalibainishwa jana jijini hapo na Meya wa Jiji hilo, Dk Didas Masaburi kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, lililokutana kwa ajili ya kuvunjwa rasmi kwa baraza hilo, kama ambavyo sheria ya kuundwa kwake inavyoelekeza.
Katika kikao hicho kilichowakutanisha wajumbe wa baraza hilo, Meya wa jiji hilo alisema moja ya changamoto zinazolikabili jiji la Dar es Salaam ni muundo wake ambao kisheria unaingiliana na mamlaka nyingine kiutendaji, hivyo kukosa nguvu ya kutekeleza majukumu yake.
“Ni kweli jiji letu lina tatizo la kimuundo, ambalo linasababisha jiji kukosa nguvu za kisheria kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake na hivyo linaonekana halifanyi kazi, ni vyema serikali ikaona sasa haja ya kuliduka upya kimuundo”,Dk Masaburi.
Awali wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Wilson Kabwe alielezea mafanikio ya jiji hilo kwa kipindi cha miaka mitano ya uwepo wa baraza hilo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kisasa vya mabasi ya mikoani cha Mbezi Louis na Boko Basihaya pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Aidha alisema miradi kadhaa iko kwenye hatua za utekelezaji kama mradi wa uendelezaji makazi kwenye viwanja vitatu tofauti katika maeneo ya Kinondoni na Oysterbay jijini hapo.
Pamoja na mafanikio hayo, Kabwe alisema zipo changamoto kama ambavyo Meya ya jiji hilo alivyoeleza na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hujikuta wakishindwa kwa kuwa maeneo ya utekelezaji yako kwenye mamlaka nyingine kama vile Manispaa, na wakati mwingine huitaji kibali kutoka kwenye Manispaa husika.
Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam liliundwa Januari 7, mwaka 2011.
CHAPAKAZI
Mgombea Ubunge Jimbo la Njombe Kusini, Rose Mayemba ambaye anagombea Jimbo ambalo lilikuwa la Spika Anne Makinda juzi alimkuta nyoka amejiviringisha kwenye siti ya abiria kwenye gari yake wakati akiwa Hotelini Njombe.
Nyoka huyo alikutwa kwenye siti kama abiria anayesubiri dereva aingie awashe gari waondoke, Mbunge huyo alikuwa kwenye Hoteli ambayo walikutana na Viongozi wa CHADEMA.
Mayemba ambaye ni Mtunza Takwimu Mkuu wa CHADEMA Wilaya ya Njombe alisema baada ya kuingia kwenye gari yake aina ya RAV 4 alishangaa kuona kitu kimejiviringisha kwenye siti ya mbele.
“Nilipokiona hicho kitu wazo la haraka nikajua ni mkanda wa abiria ambaye nilikuwa nimembeba ameusahau… nilipoona ni nyoka anataka kujiviringisha mkononi nilitoka mbio kwenda kuwaita wenzangu” >>> Rose Mayemba.
Mgombea Ubunge huyo amesema hajui nyoka aliingiaje kwenye gari lake na hawezi kumlaumu mtu ila safari yake Bungeni anamtegemea zaidi MUNGU na hatishiki na chochote.
CHAPAKAZI
Maafisa toka Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA waliokuwa katika Operesheni ya kukagua maduka ya dawa katika Manispaa ya Temeke wanadaiwa kuomba wapewe Tshs. 500,000 kutoka kwa mmiliki wa duka ili wasilifungie duka hilo.
Mwenye duka huyo Suleiman Vuai amesema maafisa hao walifika dukani kwake na kujitambulisha kuwa wanatoka TFDA lakini walisema hawakutembea na Vitambulisho vyao.
Vuai anasema baada ya kukagua duka lake walimwambia lina mapungufu ikiwemo kuiibia Serikali Milioni nane hivyo anatakiwa atoe pesa hizo vinginevyo wanachukua dawa zote zilizopo dukani.
Alipojibu kuwa hana kiasi hicho cha pesa kulitokea vuta nikuvute na baadae walimtaka awape pesa ya daku kwa kuwa wao ni Waislamu wamefunga, akawajibu kuwa hana labda awape 50,000 kama nauli.
Vuai amesema baada ya majadiliano maafisa hao waliondoka na kuahidi kurudi baadae kwa ajili ya kupatiwa 500,000 na baadae wakaendelea kumpigia simu wakiulizia waje muda gani kuchukua pesa hiyo.
Msemaji wa TFDA amesema hakuna watu walioagizwa kufanya Oparesheni yoyote na hao sio maofisa wa Mamlaka hiyo.
MTANZANIA
Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Joshua Nassar, amenusurika kifo baada ya kupata ajali ya helkopta wakati akiwa katika ziara kuhamasisha wananchi wa jimbo lake kujindikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
Afisa habari wa CHADEMA Tumaini Makene alisema ajali hiyo ilitokea jana jioni katika eneo la Leguruki na taariza za awali ni kwambwa watu waliokuwa kwenye helkopta hiyo wamepata majeraha madogo madogo.
Kwenye ndege hiyo walikuwepo viongozi wengine wa ngazi ya jimbo ambapo wao pamoja na Nassari walipelekwa hospitali ya Seliani kwa matibabu zaidi.
Taarifa zinasema helkopta hiyo ambayo inamilikiwa Mbunge Philemon Ndesamburo inasemekana chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali.
Chanzo: Millardayo.com
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.