Watu watano katika Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wamenusurika kifo baada ya kuangukiwa na kifusi wakati wakiwa kwenye maandalizi ya kujenga jengo lililotegemewa kuwa na ghorofa saba, eneo la Nyerere Road, jana majira ya saa sita mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Kunisaga alisema kuwa amesikitishwa na tukio hilo ambapo watu hao wameangukiwa na ukuta wakati wakijenga msingi wa jengo hilo na hii ni kutokana na kuwa na wakandarasi ambao hawajengi majengo kwa kiwango kinachotakiwa.
Katika hatua nyingine, Kunisaga amesema kuwa hali ya Watanzania kuwa wanapoteza uhai wao kila kukicha kutokana na kuangukiwa na vifusi, serikali haiwezi kukubaliana nayo hivyo amesitisha ujenzi wa jengo hilo.
Majeruhi waliokumbwa na tukio hilo wameongea na waandishi wa habari japo kwa taabu na kusema kuwa ukuta uliowaangukia ulikuwa umeunganishwa kama uzio hivyo wakati wakiendelea kuchimba msingi, uzio huo ulikuwa ukiendelea kutitia hivyo kusababisha kuporomoka na kuwaangukia.
Daktari wa zamu wodi ya dharura, Ernest Elisenguo amethibitisha kupokea majeruhi watano ambao wametokana na tukio la kuporomokewa na kifusi na kuwataja kuwa ni Ramadhan Hussein Nyarandu, Rashid Mkumba Hamis, Elias Bahati, Benson Agustino na Mtani ambapo watatu kati ya hao hali yao imeendelea vizuri na wameruhusiwa kwenda nyumbani ila wawili kati yao bado hali zao siyo nzuri na wataendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Majeruhi Rashid Mkumba Hamis, ameeleza kama ifuatavyo: "Mimi ni fundi na nilikuwa natengeneza 'bezi' kwa ajili ya kushikilia nguzo za ghorofa wakati ninaendelea na kazi yangu nikaanza kusikia udongo ukiniangukia mgongoni, ghafla nikasikia matofali yananiangukia.
"Katika kujiokoa matofali yakawa yameniangukia kwenye miguu na bahati mbaya kwa mujibu wa madaktari ni mwamba nimevunjika mguu ila namshukuru mungu kuona niko salama."
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.