Rais Jakaya Kikwete amekabidhiwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka unaoishia Juni 2014 na kuagiza vyombo vya dola kuwabaini maofisa wote wa Serikali wanaohusishwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Pia, Rais Kikwete ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa maofisa wote wa Serikali ambao wanahusika katika kulipa mishahara hewa kwa watumishi ambao wameacha kazi, wamefariki dunia au wamestaafu lakini wanaendelea kulipwa kupitia akaunti zao za benki.
Rais ametoa maagizo hayo jana baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo na CAG Profesa Mussa Assad. Aliiomba ofisi hiyo kuisaidia Serikali kuboresha mfumo wa zabuni kwani Serikali inapoteza fedha nyingi kwa kupitia mchakato mrefu wa kupatikana kwa wazabuni wa kutoa vifaa na huduma kwa Serikali.
“Naagiza kuwa tutume ujumbe wenye nguvu za kutosha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Serikali.”
Ukaguzi huo umebaini upungufu mbalimbali katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile malipo yasiyokuwa na nyaraka, hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha iliyotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Profesa Assad amemweleza Rais Kikwete kuwa ofisi yake inapendekeza kuwa taasisi zote za Serikali zisiendelee kununua vifaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za stakabadhi za kielektroniki (EDF).
Kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, Profesa Assad alimwambia Rais Kikwete kuwa ukaguzi wake umebaini kuwa mishahara ya watumishi waliocha kazi, waliofariki dunia na waliostaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao.
Vilevile, fedha za makato ya mishahara ya wafanyakazi hao zimeendelea kupelekwa kwenye taasisi husika kama vile Bima ya Taifa ya Afya, Mamlaka ya Mapato na mifuko ya hifadhi ya jamii.”
Profesa Assad alisema tatizo hilo linaendelea kuwapo hata kama linapungua kwa sababu ya mfumo wa udhibiti ambao Serikali imeanzisha na kuwa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2014, kiasi cha Sh141.4 bilioni kilitumika kulipa watumishi hao hewa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.